Tuesday, April 16, 2013

KWA HIYO TUAMINI KUWA ULIMBOKA ALITEKWA NA MTU MMOJA?

 



USIKU wa kuamkia Juni 26, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, alitekwa na watu wasiojukikana kisha kumpiga na kumjeruhi vibaya na kumtelekeza katika Msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Dk. Ulimboka alitekwa zikiwa ni siku tatu baada ya mgomo wa madaktari kuanza. Alikuwa na wenzake eneo la Leaders Club Wilaya ya Kinondoni.
Ni takriban miezi 10 tangu Dk. Ulimboka atekwe na kuteswa lakini ni mtuhumiwa mmoja pekee, Joshua Mulundi, ndiye ameshtakiwa kutokana na tukio hilo.
Tunatambua utaratibu wa Jeshi la Polisi kuwa suala hilo bado linaendelea kupelelezwa, lakini hoja yetu ni kwamba Dk. Ulimboka alitekwa na kuteswa na mtu mmoja?
Hofu yetu inatokana na jinsi tukio hilo linavyofanyiwa kazi. Dk. Ulimboka mwenyewe licha ya kutamka hadharani kuwa alitekwa na watu zaidi ya watatu na hata wengine kuwataja kwa majina, Jeshi la Polisi halijamhoji. Kuna siri na ajenda gani hapa?
Masuala ya utekaji na utesaji katika taifa letu yanaanza kuwa ya kawaida kwani baada ya tukio la Dk. Ulimboka na sasa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, alifanyiwa unyama kama huo usiku wa Machi 6, mwaka huu.
Kwa mantiki ya kawaida, ni jambo la kushangaza kuona tangu tukio la Ulimboka lifanyike, ni mtuhumiwa mmoja pekee amefikishwa mahakamani, tena bila kukamatwa na Jeshi la Polisi bali alifikishwa huko baada ya walinzi wa kanisa moja kutilia shaka akili yake.
Dk. Ulimboka alikamatwa kwa nguvu na watu zaidi ya mmoja, akaingizwa kwenye gari kisha akapelekwa kusikojulikana na kufanyiwa unyama huo na baadaye akatelekezwa.
Je, haya yote yalifanywa na mtu mmoja pekee? Jeshi la Polisi kwa miezi 10 liko wapi? Ni kwanini limeendelea kupiga danadana katika suala hili?
Jeshi la Polisi linapaswa kumaliza utata huu kwa kumhoji Dk. Ulimboka na watuhumiwa wengine wote aliowataja kuhusika na kuteswa kwake ili liweze kujirejeshea uaminifu wake kwa raia.
Itaendelea kutia shaka endapo kesi ya mtuhumiwa Mulundi itabaki kupigwa kalenda kwa kisingizio cha upelelezi wa tukio hilo kuendelea kumbe hakuna watuhumiwa wengine wanaosakwa.
Tunasema hivyo kutokana na jeshi hilo makao makuu kutoa kauli za kukinzana na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Februari mwaka huu, Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, aliliambia gazeti hili kuwa sakata la Ulimboka halikuundiwa kamati ya kulichunguza na kwamba hata hivyo hayo ni mambo ya mwaka jana, sasa wameingia mwaka mpya.
Wakati Senso akisema hivyo, Kova alisema kamati hiyo iliyoundwa kuchunguza suala hilo ilimaliza kazi yake na kuwasilisha ripoti katika ngazi ya juu na baadaye IGP Said Mwema alisema sakata la Ulimboka ni siri ya taifa.
Kwa kauli hiyo ya Mwema, ni wazi kuwa hakuna kinachoendelea tena katika sakata la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka. Hivyo yafaa umma ukafahamu kama alitekwa na mtu mmoja pekee.