Msanii atumia noti kutengeneza ndege za kuchezea watoto
"Aonyesha sanaa zake hadharani kwenye kipindi cha Televisheni"
"Benki Kuu yamuonya vikali
PESA hukosa
thamani lakini heshima yake hulindwa na kubakia palepale. Pesa
zinapokosa thamani kiasi cha noti kutumika kuchambia chooni na
kutengeneza ndege za kuchezea watoto basi hapo tena ni makubwa.
Watu wote walioketi karibu na televisheni zao jijini
Brasilia mji mkuu wa Brazil hawakuamini macho yao kuona msanii
aliyebobea kwa kuonesha michezo ya watoto akitumia noti za pesa ya nchi
yao "Cruzeiro"kutengeneza ndege za kuchezea watoto kisha kuzionesha
kwenye kipindi cha televisheni ya taifa .
Tukio hilo la aina yake siyo kuwa liliwaacha hoi
wananchi wa Brazil peke yao, bali hata Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo
alichukuwa hatua za kuwasiliana na msanii huyo kwa njia ya simu papo
hapo.
Silvio Santos ni msanii anayeheshimika sana nchini
Brazil na aliyejizolea sifa kemkem, amelitangaza jina la Brazil hata nje
ya mipaka ya nchi hiyo.
Kwa mantiki hiyo, hakuna aliyetarajia kuwa Santos
angelifedhehesha nchi yake kiasi hicho. Kwa kuheshimu mchango wa Santos
katika sanaa nchini humo, Gavana wa fedha alimwambia aache mara moja
utovu wake wa nidhamu vinginevyo wangelimchukulia hatua kali mara moja.
Lakini Mac. Margolis mwandishi anayeandikia jarida
mashuhuri Brazil la "Veja Journal", anasema kuwa ‘watu hawa wanamuonea
Santos tu’
Mwandishi huyo anasema kuwa uchunguzi alioufanya
kwenye mitaa mbalimbali ya Brasilia hususan maeneo ya madogo, wananchi
walijawa na ghadhabu kufuatia kushuka sana kwa thamani ya pesa yao na
sasa hawaithamini tena pesa hiyo inayoitwa "Cruseiro"
alishuhudia walevi kwenye vilabu vya usiku
vichochoroni wakitumia pesa hiyo kwa kuchambia chooni; akina mama
wanaouza bidhaa walitumia noti hizo kuwafungia wateja wao bidhaa
walizonunua na hata watu wengine wakizitumia kufuta vumbi kwenye
madirisha ya nyumba zao na mbaya zaidi ni wauzaji wa madawa ya kulevya
aina ya "Cocaine" ambao wanatumia pesa hiyo ya Brazil kufunga madawa
hayo ya kulevya.
Je, ni kwa nini "Cruzeiro" idharaulike kiasi hicho?
Wachunguzi wa mambo kwa karibu huko Brazil wanasema thamani ya pesa ya
nchi hiyo imeshuka kiasi kwamba ilifika wakati mmoja ambapo pesa ya
Brazil ingeliweza kushindanishwa thamani yake na pesa ya Jamuhuri ya
Kidemorasia ya Congo Kinshasa na pesa ya Bosnia peke yake. kiwango cha
kushuka kwa pesa ya Congo Kinshasa inajulikana kwani katika nchi hiyo
baada ya kifo cha Hayati Joseph Mobutu Seseseko Kuku wa Zabanga wakazi
wa kijiji anachotokea cha Gbadolite wamekataa kutumia pesa mpya ya
serikali ya sasa badala yake wanatumia ile ile ya wakati wa Mobutu.
Kwenye mtaa mmoja wa mji mkuu wa Brazil wa Brasilia,
mwanamke muuzaji wa bidhaa ametandaza makaratasi lukuki na sarafu zisizo
idadi hakika huwezi kutofautisha ipi ni pesa na ipi ni bidhaa.
Kwani noti za "Cruzeiro"zimelaliana kiasi cha kuwekwa katika mafungu mafungu mithili ya nyanya.
Nako vichochoroni unakopita penye mitaa ya miji
mikubwa ya Brazil kama Rio-de-janeiro na Salam siyo jambo la ajabu kwa
wakazi wa huko kukutana na noti za "Cruzeiro"zilizotupwa mithili ya
takataka.
Bei za bidhaa ikiwemo vyakula hupanda maradufu
karibia kila mwezi nchini humo. Wapo wafanyabiashara ambao sasa wameacha
kutumia "Cruzeiro"na badala yake wanatumia Dola za Kimarekani na Paundi
ya Uingereza peke yake.
Mtu anayeenda kununua shati moja dukani huko Brasilia, hana budi kubeba kikapu kizima cha noti.
Ni katika hali hiyo ndiyo msanii Silvio Santos;
liwalo na liwe akaamua kuithibitishia serikali yake kuwa ni kwa kiasi
gani pesa yao ni feki.
Naye akaona yafaa kutengeneza ndege za watoto tu.